KHADIJA MKE WA MTUME 4
Baada ya kupatwa na misiba miwili hiyo,
(kufiwa na mumewe wa pili na kufiwa na baba yake) Bibi Khadija (Radhiya Llahu
anha) aliishi akiwa mwingi wa huzuni na mwingi wa kutafakari. alijitenga mbali
na watu na aliacha hata kwenda kutufu Al Kaaba kama alivyokuwa akifanya hapo mwanzo.
Inajulikana kuwa Bibi Khadija (Radhiya Llahu
anha) hakupata hata siku moja kuyasujudia masanamu yaliyokuwepo hapo, na hii ni
siri aliyomjulisha bin ami yake maarufu Waraqah bin Noufel aliyekuwa akifuata
dini ya Manasara.
Waraqah bin Noufel huyu alikuwa mcha Mungu
sana na alikuwa akisoma sana vitabu vilivyotangulia na kwa ajili hiyo alikuwa
akijulikana sana miongoni mwa waarabu wa Makka kwa ucha Mungu wake na wema
wake.
Siku moja Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha)
akiwa na uso uliojaa huzuni alikwenda kumtembelea bin ami yake huyo
aliyemuuliza:
“Kuna nini binti ami yangu, mbona nakuona una
huzuni nyingi?”
Bibi Khadija akamwambia:
“Sijaiona tena furaha tokea alipofariki baba
yangu, na mali nyingi niliyoirithi haikuweza kuziba pengo lake”.
Waraqah akamwambia:
“Usihuzunike ewe binti ami yangu, utakuja
kuonana naye Akhera”.
Bibi Khadija akashangaa:
“Akhera? Ni kitu gani hicho kinachoitwa akhera
ewe bin ami yangu?”
Waraqah:
“Hayo ni maisha baada ya kifo, na katika
maisha hayo kila nafsi itapata jaza yake kutokana na yale yaliyotanguliza
mikono yake”.
Bibi Khadija akauliza huku akitetemeka:
“Ina maana kuwa baba yangu hivi sasa yuhai?”
Waraqah akamwambia:
“Ndiyo, roho yake iko hai, isipokuwa mwili
wake ushachanganyika na udongo wa ardhi”.
Bibi Khadija akaanza kusema huku mwili wake
ukiwa unamtetemeka:
“Bin ami yangu, nataka kukupa siri
niliyoizuwia moyoni mwangu tokea nilipokuwa mtoto mdogo mwenye umri wa miaka
sita”.
Waraqah akasema:
“Sema ewe binti ami yangu wala usiwe na
khofu”.
Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) akasema:
“Nilipokuwa na umri wa miaka sita hivi,
nilikwenda siku moja pamoja na baba yangu penye Al Kaaba nikamuona akisimama
mbele ya masanamu yaliyotengenezwa kwa mawe kisha anayakabili na kukiinamisha
kichwa chake kwa kuyaheshimu. Nikamuuliza:
“Nini haya masanamu ewe baba yangu?”
Akaniambia:
“Hii ni miungu tunayoiabudu”.
Nikashangazwa nikiwa bado mdogo, vipi watu
wanayaabudu mawe yasiyoweza kudhuru wala kunufaisha?”
Waraqah akamtizama Bibi Khadija (Radhiya Llahu
anha) huku akitabasamu, kisha akamwambia:
“Uliwahi kumhadithia mtu yeyote katika watu wa
nyumbani?”
Bibi Khadija akasema:
“Abadan, abadan. Sijapata kumhadithia mtu
yeyote, kwani nilikuwa nikiogopa sana, nikaificha siri hii mpaka nilipokuja
kukuhadithia wewe sasa hivi. Nini rai yako ewe bin ami yangu?”
Waraqah akamwambia:
“Huo ndio ukweli wenyewe. Yale
ni mawe tu yasiyodhuru wala kunufaisha. Na atatokea katika zama zetu hizi Mtume
anayesubiriwa atakayeyavunja masanamu haya na kuondoa ushirikina na uonevu
katika ardhi”.
Bibi
Khadija (Radhiya Llahuu anha) akauliza:
“Na
lini atakuja Mtume huyo?”
Waraqah
akasema:
“Mwenyezi
Mungu ndiye Anayejuwa zaidi, isipokuwa vitabu vinasema kuwa; atatokea Mtume
katika wakati huu wetu na yeye ndiye atakayekuwa mwisho wa mitume”.
Bibi
Khadija akauliza:
“Na
katika kundi lipi atatokea mtume huyo?”
Waraqah
akasema:
“Allahu
aalam, lakini Mayahudi wanasema kuwa atakuwa katika wao, na vitabu vinasema
kuwa atakuwa miongoni mwa Waarabu”.
Bibi
Khadija:
“Na
uliyajuaje yote haya ewe bin ami yangu?”
Waraqah:
“Haya
yameandikwa katika Tuarati kitabu cha Mayahudi na katika Injili kitabu cha
Manasara”.
Bibi
Khadija akaondoka hapo huku mawazo yake yote yakiwa juu ya huyo Mtume mpya
aliyebashiriwa na bin ami yake atakayeuondoa ushirikina na dhulma na jeuri
iliyopindukia mipaka, lakini wakati huo huo mazungumzo hayo yalimsaidia sana
katika kupunguza uzito uliokuwepo kifuani pake na huzuni aliyokuwa nayo, na kwa
ajili hiyo akaanza tena kufanya shughuli zake za kawaida pamoja na za
kibiashara.
No comments