KHADIJA MKE WA MTUME 3
Haukupita muda mrefu bibi Khadija (Radhiya
Llahu anha) akaolewa na Nibash bin Zirarah Al Tamimi aliyekuja kujulikana kwa
jina la ‘Abu Halah”, na wakapata watoto wawili waliowapa majina ya
Hind na Halah.
Waliishi kwa wema mpaka mumewe wa pili naye pia alipofariki
dunia, na haukupita muda mrefu baba yake Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) naye
pia akafariki dunia, jambo lililozidisha huzuni moyoni mwake. (zipo riwaya
zinazosema kuwa baba yake bi Khadija alifariki dunia baada ya binti yake
kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Laahu alayhi wa sallam) na kwamba
yeye ndiye aliyeifunga ndoa yao. Hata hivyo riwaya zenye nguvu zaidi zinasema
kuwa alifariki kabla ya bibi Khadija kuolewa na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla
Laahu alayhi wa sallam) na kwamba aliyefunga ndoa ya bibi Khadija na Mtume
(Swalla Laahu alayhi wa sallam)alikuwa kaka yake anayeitwa Amru bin Khuwaylid.
Baada ya misiba hiyo iliyofuatiliana, Bibi
Khadija aliyerithi mali nyingi sana kutoka kwa baba yake na kutoka kwa waume
zake waliofariki, aliamua kujitenga na watu akawa anajishughulisha na ulezi wa
wanawe.
Watu wengi walipeleka posa kutaka kumuoa,
lakini Bibi Khadija (Radhiya Llahu anha) aliwakataa kwa sababu alihisi kuwa
wote hao walikuwa wakimtaka kwa ajili ya tamaa ya mali yake na uzuri wake.
No comments